UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umewafukuza wanafunzi 13 na kumsimamisha masomo kwa muda usiojulikana Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso), Kilawa Simon na wenzake 85, kwa kuchochea na kushiriki mgomo uliovuruga utaratibu wa masomo chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana, kwamba ulifikiwa juzi kwa kuzingatia maazimio ya mkutano wa 206 wa Baraza la Chuo Desemba 13, mwaka jana, unaokataza uvumilivu kwa wanafunzi wasiotii na kuheshimu sheria za chuo hicho.
Miongoni mwa waliofukuzwa na kukabidhiwa barua zao jana ni Spika wa Bunge la Wanafunzi, Peter Anold na mawaziri wa Daruso; Naftal Daniel (Mikopo), Mwakyusa Daniel na Naibu wake Masiga Gulatone (Taaluma). Wamo pia viongozi wengine tisa wa Serikali hiyo pamoja na Wilfred Bocasa wa mwaka wa pili asiye na wadhifa.
Wakati Mukandala akisisitiza kuwa kufukuzwa huko hakukuzingatia nyadhifa za wanafunzi hao bali makosa yao, imeelezwa kuwa idadi kubwa ya waliopewa adhabu hiyo ni viongozi, wakiwamo mawaziri na wabunge ambao kwa namna moja au nyingine walihamasisha au kushiriki mgomo huo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mukandala alisema uamuzi huo ni sahihi kulingana na makosa yaliyofanywa na walioadhibiwa, na kwamba huenda idadi ya watakaofukuzwa ikaongezeka au kubaki ilivyo, kulingana na matokeo ya uchunguzi unaoendelea kwa waliosimamishwa.
“Waliofukuzwa wamebainika kuhusika moja kwa moja na uchochezi na ushiriki wa mgomo uliotokea jana (juzi) na kuvuruga shughuli za masomo chuoni hapa. Kwa kuwa kitendo hicho ni batili, uchunguzi ulifanywa na kuwabaini vinara 13 waliopewa barua zao leo (jana).
“Waliosimamishwa wanaendelea kuchunguzwa na endapo watabainika vinara wengine chuo hakitasita kuwafukuza na kuwarejesha darasani watakaoonekana kutohusika. Haki itazingatiwa na hakuna atakayeruhusiwa kuingia darasani hadi uchunguzi utakapokamilika na chuo kutangaza vinginevyo,” alisema Mukandala.
Alitaja chanzo cha mgomo huo kuwa ni kuushinikiza uongozi wa chuo hicho uwarejeshe masomoni bila masharti, wanafunzi 48 waliofukuzwa na Baraza la Chuo pamoja na wanne waliosimamishwa Desemba 14 mwaka jana, kwa kukiuka sheria za chuo.
“Baadhi ya wanafunzi wanaponzwa na mashinikizo ya viongozi wao na kukaidi sheria na utaratibu wa chuo. Migomo inafanywa na wachache kwa kushinikizwa na viongozi wasiopenda kutii maagizo ya Baraza na uongozi wa Chuo, ndiyo maana hata huu wa sasa umefanywa na baadhi ya wanafunzi na wala si wote.
“Kwa kuwa waliamua wenyewe kushiriki mgomo, chuo hakitafungwa ili kutoa nafasi kwa wanafunzi waliokuja kusoma waendelee na masomo yao, huku ulinzi wa FFU (Polisi wa Kuzuia Ghasia) ukiwa mahali hapa kuhakikisha kuwa hawabughudhiwi,” alisema Mukandala.
Kwa maelezo ya Mukandala, wanafunzi waliofukuzwa pamoja na waliosimamishwa masomo, waliamua kupinga uamuzi halali wa Baraza la Chuo hicho wa kuwafukuza wenzao, kwa kushinikiza na kushiriki mgomo huo, huku wakijua kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania ndiyo pekee, yenye uwezo wa kutengua uamuzi wa Baraza hilo na si mgomo wala vurugu.
“Licha ya wanachuo kufahamu maazimio ya Baraza, baadhi yao waliendelea kukaidi kwa kushinikizwa na viongozi wao wanaofanya uchochezi wa migomo. “Januari 7, wabunge wa Bunge la Wanafunzi wakiongozwa na Spika wao walifikia uamuzi batili wa kuhoji na kushawishi mgomo kupinga uamuzi wa Baraza wa kuwafukuza wenzao,” alisema Mukandala.
Alisema hata baada ya kupewa onyo Januari 8, viongozi hao waliendelea kukaidi kwa kusisitiza mgomo ambapo Daruso ilitoa msimamo wake wa kutaka uamuzi wa Bunge hilo utekelezwe na hivyo kubariki mgomo huo kwa mikono miwili.
Juzi baadhi ya wanafunzi walionekana wakizunguka katika barabara za chuo hicho Mlimani wakiwa wamebeba mabango na kuimba kuwa hawataingia madarasani bila wenzao kurejea chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment