Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Idd amewataka wananchi wa Zanzibar kwa pamoja waijadili Sheria ya adhabu ya kifo nakudai kuwa si jambo la busara kuachiwa wasomi peke yao kujadili sheria hiyo.
Amesema wananchi wa Zanzibar kwa umoja wao wanapaswa kuijadili sheria hiyo kama inafaa au haifai na si vyema wasomi wakaachiwa peke yao kuijadili sheria hiyo ambayo utekelezaji wake umekuwa mgumu kufanyika katika mataifa mengi.
Balozi Idd ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya kuunga mkono tamko la Umoja wa Mataifa juu ya adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Eacrotanal mjini Zanzibar.
Amesema adhabu ya kifo ambayo imehalalishwa katika vitabu vitakatifu vya Kuran na Agano la Kale imekuwa ikipata changamoto nyingi kutokana na ugumu wa utekelezwaji wake jambo ambalo hupelekea wanaharakati wengi kupinga uhalali wake.
Aidha amewataka wasomi wa Zanzibar wenye uwezo wa kuandika kuendelea kuandika vitabu na machapisho mbali mbali yanayohusu Zanzibar jambo ambalo litaipandisha hadhi Zanzibar.
Amesema si vyema kwa mambo ambayo yanatokea katika ardhi ya Zanzibar kuandikiwa na wasomi kutoka nje ya Zanzibar jambo ambalo hupelekea kasoro nyingi za ushahidi.
Maadhimisho hayo pia yalitoa fursa kwa Balozi Seif kuzindua rasmi vitabu viwili ambavyo vipo chini ya udhamini wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar.
Vitabu vilivyozinduliwa ni pamoja na “Adhabu ya Kifo katika Sheria za Kiislamu” kilichotungwa na Dk. Muhyiddin Ahmad Khamis na “Zanzibar the Development of the Constitution” ambacho kimehaririwa na Prof. Chris Maina.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia Viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abuubakar Khamis, Wanasheria, Mawakili, mashekh na wadau mbalimbali wa Zanzibar. |
No comments:
Post a Comment