KUNA kila dalili ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine mdogo kwa upande wa Tanzania Bara, baada ya mbunge wa NCCR-Mageuzi Jimbo la Mhambwe, Felix Mkosamali kuanza mazungumzo na Chadema kwa lengo la kutaka kuhama chake cha sasa. Tayari taifa lilishuhudia uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika Oktoba mbili kujaza nafasi ya Rostam Aziz aliyejiuzu nyadhifa zote ndani ya CCM ikiwamo na ubunge kwa madai kuwa chama chake kinaendesha siasa za uchwara. Wakati uchaguzi huo wa Igunga ukitajwa kutumia rasilimali nyingi za vyama vya siasa ikiwamo mabilioni ya fedha, Mkosamali ambaye ni mbunge kijana wa NCCR-Mageuzi anatajwa kufanya mazungumzo na Chadema na huenda akatangaza kujiuzulu wadhifa huo na unachama wa chama chake cha sasa wakati wowote.
Kwa mujibu wa washirika wa karibu wa Mkosamali, uamuzi huo unatokana na kile kinachoelezwa ni msuguano wake wa chini kwa chini na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Washirika hao wa karibu wa Mkosamali, walifafanua kwamba msuguano huo umemfanya mbunge huyo kufikiria uamuzi huo wa kuhama chama chake na kujiunga Chadema ambako anaamini anaweza kutimiza malengo yake kisiasa. Hata hivyo, alipoulizwa mwenyewe kwa njia ya simu, alijibu kwa kifupi, "Kaka una haraka gani? Si unisubiri kesho (leo) unipigie? Kesho nitakwambia kila kitu. Kwanza nani kakupa hizi taarifa,? Aliuliza Mkosamali
Naye rafiki yake wa karibu Metusela Mawazo aliiambia Mwananchi kwamba naye amesikia taarifa za Mkosamali kutaka kuhamia Chadema kutokana na hali inayoendelea ndani ya NCCR-Mageuzi. “Kimsingi nimezipata taarifa za Mkosamali kuanza harakati za kuhamia Chadema, zimenistusha sana. Ni taarifa za kweli na kama unavyojua mwananchi yoyote anaweza kuhamia chama anachokitaka,” alisema Mawazo. Alisema kwa jinsi anavyomjua Mkosamali kimsimamo hayuko tayari kufanya kazi akiwa NCCR-Mageuzi. “Ni rafiki yangu wa karibu sana, hayuko tayari kufanya kazi akiwa NCCR-Mageuzi, ni mpambanaji na nina uhakika atashinda uchaguzi mdogo,” alisema Mawazo ambaye aligombea ubunge kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi Jimbo la Buyungu Kibondo na kuchuana vikali na mgombea wa CCM, Christopher Chiza.
Mbatia akana msuguano
Hata hivyo, Mbatia alipoulizwa kuhusu hilo, alistuka huku akisema, ''Mimi sina msuguano na Mkosamali kwani hata juzi tulikuwa naye kwenye kikao. Tulifanya nae kikao na tukazungumza vizuri tu, hilo la msuguano ndiyo nasilikia kwako".
Mbatia alisema mwisho jana, aliwasiliana na Mkosamali ambaye alimtumia ujumbe mfupi wa simu akimwomba mwenyekiti huyo afuatilie vema kuhusu kesi yake ya jimbo la Mhambwe na kutaka chama kilijadili vema.
"Sasa nashangaa unavyoniambia anataka kuhama au nina msuguano nae. Leo (jana) alinitumia ujumbe mfupi kuhusu kesi ya uchaguzi jimbo lake la Mhambwe. Alitaka chama kijadili vema hilo na nikamwambia sawa," alisema Mbatia.
Hata hivyo, vyanzo zaidi vilivyo karibu na Mkosamali vilidokeza jana usiku kwamba Mbatia ameomba kukutana na mbunge huyo leo kwa ajili ya kujadili zaidi suala hilo ambalo linaweza kuwa pigo kuu kisiasa kwa NCCR-Mageuzi. NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kilipata viti vinne vya majimbo ambavyo ni Kigoma Kusini kwa David Kafulila, Mhambwe kwa Mkosamali, Kasulu Vijini Zaitun Buyogela na Kasulu Mjini kwa Moses Machali. |
No comments:
Post a Comment