Leo, Desemba 9, 2010, nchi yetu itaadhimisha miaka 49 ya Uhuru. Ndiyo, miaka 49 ya Uhuru; yaani tumebakiza mwaka mmoja tu tutimize nusu karne tangu tulipojikomboa kutoka kwenye minyororo ya ukoloni.
Katika miaka hiyo 49 ya Uhuru, yametokea mabadiliko mengi makubwa ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na hata kifikra. Mengi ya mabadiliko hayo ni chanya, na hivyo tunapaswa sote kujipongeza; lakini yapo machache ambayo ni hasi na hatari zaidi kwa ustawi wa taifa letu. Hayo ndiyo tunayopaswa sote kuyapigia kelele.
Moja kubwa lililo dhahiri ni kuporomoka kwa umoja wetu; tatizo linaloendana pia na kuporomoka kwa uzalendo. Tatizo hili tusipolitatua litaibua matatizo mengine mengi na makubwa ambayo, hatimaye, yatalisambaratisha kabisa Taifa la Tanzania, na pengine kuliingiza katika umwagaji damu.
Labda tukumbushane tu kwamba Umoja wa Watanzania uliojengwa na mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere, ulikuwa wa kihistoria, na misingi yake ni katika mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, na zaidi ya yote unyonywaji wa wananchi.
Umoja huo ulitokana na imani ya uwezekano wa ujenzi wa jamii yenye haki, usawa na heshima kwa kila mtu bila kujali jinsia, rangi au kabila.
Tujiulize: Miaka 49 baada ya Uhuru, hali ikoje sasa? Si siri kwamba hivi sasa kuna nyufa nyingi mno katika Umoja wetu, na haishangazi kwamba sasa Watanzania huzungumzia udini, ukabila, ukanda nk, mambo ambayo huko nyuma hayakuwepo kabisa.
Ni kwa nini Umoja wetu unasambaratika kwa kasi? Yapo majibu mengi kwa swali hilo, lakini jibu kuu ni kwamba watawala wetu wameachia kupanuka kwa kasi kwa pengo kati ya Walionacho na Wasionacho; hali ambayo imeimarisha matabaka.
Si siri kwamba hali hii imeongezeka zaidi baada ya watawala wetu kuitosa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na pia kujitumbukiza katika mfumo wa biashara wa soko huria; mambo ambayo kwa pamoja yamejenga nchini mwetu watawala na wanasiasa wenye mitazamo ya u-mimi badala ya utaifa, na pia wenye ulafi na tamaa ya kupindukia ya kujilimbikizia mali.
Tukumbuke kwamba Umoja wetu ulitokana na imani kwamba inawezekana kujenga jamii isiyo na nafasi ya mazingira yanayowafanya watu wengi kulala njaa; huku wachache wakila na kusaza, wengi wakiishi kwenye nyumba za udongo na wachache wakiishi kwenye ‘mahekala’ ya kifahari. Hakika, ni vigumu Umoja kuendelea kushamiri katika mazingira kama hayo.
Hivyo; tunaposherehekea (kesho) miaka 49 ya Uhuru wetu; natujitazame upya, tujihoji na tutafakari kama kweli hatujapotea njia aliyotuonyesha Mwalimu Nyerere ya namna ya kujenga Taifa imara lenye kusimamia kwenye haki na usawa.
Tunawatakia nyote maadhimisho mema ya miaka 49 ya Uhuru.
No comments:
Post a Comment