To Advertise on this Blog please Call: O713 397 767 or 0785 555 560                                                 To Advertise on this Blog please Call: O713 397 767 or 0785 555 560
Mail Me

Friday, January 21, 2011

Wasomi walonga kuhusu Katiba mpya

Prof. Shivji ‘abomoa’ hoja za wanasiasa majukwaani
Asema madai ya Katiba mpya hoja si upungufu au kupitwa na wakati
Mwenzake asema jamii iliyoridhia kaulimbiu za full-kujirusha, kuchizika ni ovyo

Januari 15, mwaka 2011, Umoja wa Wanataalama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) waliandaa kongamano la Katiba. Mwandishi Wetu, Godfrey Dilunga, aliyehudhuria kongamano hilo Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salam anaeleza hapa mitazamo ya wazungumzaji wakuu, Profesa Issa Shivji na Jenerali Ulimwengu.

PROFESA Shivji ndiye aliyeanza kufungua dimba kwa kuelezea maeneo matano, akisisitiza kujenga hoja bila jazba na kusikiliza hata usiyoyakubali.
Lakini kabla, aliwapiga kijembe wanasiasa akisema; “Mimi ni mwanazuoni sio mwanasiasa ingawa napenda siasa...huwa wanasiasa hawapendi siasa wanapenda madaraka.”
Kimjadala alizungumzia sehemu tano. Mosi; maana na dhana ya Katiba. Pili; kwa nini Katiba mpya? Tatu; historia ya utungaji Katiba nchini.
Nne; mapendekezo ya mchakato wa kutunga Katiba mpya. Lakini suala la tano kwa kuwa hakuwa na uhakika wa muda akasema; nikibaki na muda nitatoa mifano ya maeneo ya kufikiriwa kuingizwa katika Katiba mpya.

Dhana ya Katiba
“Tukiwasikia wanasiasa hata wanataaluma tunaambiwa Katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Dhana hiyo chimbuko lake ni wanafalsafa, akina John Huss.
Katika kipindi cha mpito kati ya utawala wa kidikteta na kuekelea utawala wa kidemokrasia wakaibua dhana ya mkataba (social contract). Dhana hii imepitwa na wakati.
Maana na dhana ya Katiba sasa ni muafaka wa kitaifa. Katiba ni kielelezo cha muafaka wa kitaifa. Watu wamekubaliana juu ya misingi mikuu ya jamii yao, utawala wao, mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kuiweka katika Katiba.
Chimbuko la maana na dhana ya Katiba ni people sovereignty ; mamlaka yote yanatokana na wananchi wenyewe. Ndiyo maana tunasema Katiba ni mali ya jamii, kwa sababu ni yao.
Ukikubaliana na dhana hii, inakuja mantiki na sababu ya hoja kwamba; utungaji wa Katiba hauna budi kukita kwenye ushirikishwaji wa wananchi.
Kama Katiba ni mali yao, ni muafaka wao, watafikiaje muafaka huo kama wao hawakushiriki kuitunga?

Kwa nini Katiba mpya?
Kumekuwa na hoja zinatolewa na wanasiasa, wasomi na waandishi wa habari, kwa nini tuwe na Katiba mpya.
Tunaweza kuzigawa katika mafungu mawili. Kwanza, wanasema Katiba tuliyonayo ina upungufu. Wananukuu ibara mbalimbali kuonyesha upungufu.
Mtoa hoja mmoja ameorodhesha zaidi ya mapungufu 90 ya Katiba. Mimi kama mtaalamu wa Katiba, ningeweza kuorodhesha hata mapungufu 200.
Hakuna Katiba popote duniani isiyo na mapungufu. Naamini hiyo si hoja ya kuwa na Katiba mpya.
Kwa sababu kama Katiba ina mapungufu, Serikali imesema...CCM imesema kama kuna mapungufu tutayarekebisha...kuna haja gani ya Katiba mpya?

Na huwezi ukaipuuza hoja hiyo kwa sababu hoja yako ya kuwa na Katiba mpya (kama) ni mapungufu jibu lake ni kurekebisha. Na Katiba yetu ibara ya 98 inatoa uwezo kwa Bunge kurekebisha Katiba.
Katika Bunge lote la miaka 30, Katiba imerekebishwa mara 14 kutokana na mapungufu. Hoja ya pili ( ya kudai Katiba mpya) wanayotumia ni Katiba kuwa na viraka.
Neno viraka linachukiliwa kwa jazba. Katiba zote zinarekebishwa kama marekebisho ni viraka kuna ubaya gani? Katiba lazima irekebishwe ili iende na wakati.
Kundi la pili la watoa hoja wanaodai Katiba mpya ni kwamba Katiba iliyopo imepitwa na wakati. Sasa wanatoa hoja kwa nini imepitwa na wakati.
Wanasema ina miaka 30...umri wa Katiba si hoja. Katiba ya Marekani ina zaidi ya karne mbili, Katiba ya India ina zaidi ya miaka 60, na zimedumu.
Wengine wanasema imepitwa na wakati ingawa hawabainishi, maana yao ni kwamba; Katiba bado inataja sera ya Ujamaa na Kujitegemea.
Wanaozungumzia Ujamaa na Kujitegemea hawajaisoma Katiba na kuichambua. Tulipoingia katika mfumo wa neo liberalism Katiba ilirekebishwa na mara ya kwanza, katika ibara ya 151 ibara ndogo ya kwanza, iliwekwa tafsiri ya Ujamaa na Kujitegemea.
Ukisoma tafsiri hiyo ya dhana ya Ujamaa na Kujitegemea, hakuna kiongozi yeyote duniani ambaye hawezi kuwa mjamaa.

Kwa hivyo, kuendelea kutumia maneno haya (Ujamaa na Kujitegemea) wakati dhana imechakachuliwa, haina maana. Sioni kwamba hii ni sababu ya Katiba kupitwa na wakati.
Sisemi Katiba haina mapungufu, tunahitaji Katiba mpya kwa sababu tukirudi nyuma kihistoria, Katiba hii haikuwashirikisha wananchi.
Upungufu wa Katiba ya sasa ni wananchi kutoshiriki kuitunga. Uhalali wa Katiba hautegemei sana uzuri au ubaya wa ibara zake, unategemea jinsi ilivyotungwa.
Upungufu huo haurekebishiki kupitia Bunge, ndiyo maana hoja yetu ya kudai Katiba mpya haikuanza jana au baada ya Uchaguzi Mkuu, ilianza takriban miaka 20 iliyopita.
Tangu mwaka 1990 wakati Rais Mwinyi alipotangaza kuunda Tume ya maoni kuhusu chama kimoja au vingi, sisi wachache Chuo Kikuu tulisema ni wakati muafaka kuanza mchakato wa Katiba mpya.
Niliandika makala Daily News nikipendekeza mchakato wa Katiba mpya itakayokuwa na uhalali wa kisiasa na kisheria. Viongozi wakuu CCM walilaani, hawakutaka Katiba mpya.
Viongozi wa upinzani watarajiwa hawakupendezwa na mapendekezo yangu. Nilipotoa mchakato huo ambao ungekuwa wa miaka miwili, mitatu hivi nikaambiwa na mmojawapo wewe Shivji vipi, sisi tunataka kuingia Ikulu. Walikuwa na haraka ya kuingia Ikulu, hatimaye Katiba ikarekebishwa.

Historia ya utungaji Katiba
Katiba yetu ya 1977 na zilizotangulia hazikushirikisha wananchi.
Katika miaka 50 ya Uhuru tumekuwa na Katiba mpya tano. Ya kwanza ilikuwa mwaka 1961, Katiba ya Uhuru. Ilitungwa na Bunge la Uingereza, ilikuwa nyongeza katika ordering council ya kutoa uhuru kwa Watanganyika.

Katiba ya pili ilikuwa mwaka 1962, Katiba ya Jamhuri. Kulikuwa na white paper, mapendekezo ya Serikali juu ya Katiba ya Jamhuri ya 1962.
Watu walitoa maoni juu ya white paper: Kwanza walikuwa wachache, pili ni wataalamu, na tatu, ni watalaamu kutoka nje, si Watanzania.
Katiba ya 1962 ilitungwa kwa Bunge la wakati huo kujigeuza Bunge maalumu, likakaa, likapitisha sheria kujigeuza hivyo na kupitisha Katiba ya 1962.
Bunge lile lilikuwa na wabunge 71 wanachama wa TANU. Wabunge 70 waligombea uchaguzi, mmoja alikuwa mgombea binafsi (huru) marehemu Mzee Sarwatt. Wakapitisha Katiba bila ushiriki wa wananchi.
Katiba ya tatu ni ya mwaka 1964, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Chimbuko lake ni mapatano ya Muungano (articles of union).

Katiba ya kwanza ilikuwa ni Bunge la Uingereza, Katiba ya pili ilikuwa Bunge lililojigeuza kuwa Bunge maalumu, Katiba ya tatu ilitungwa na Rais.
Katiba ya nne ilikuwa ya muda ya 1965 iliyotungwa na Bunge kama sheria ya kawaida. Bunge hili halikujigeuza kuwa Bunge la Katiba, likapitisha sheria ya Katiba ya 1965.
Wakati ule hatukuwa na mjadala kuhusu hiyo lakini sasa constituency jurisprudence (falsafa na maarifa ya katiba) tumeendelea sana.
Sasa Bunge lililopo lipo kwa mujibu wa Katiba iliyopo, tuelewe hoja hiyo. Tumewachagua na kuwatuma wabunge kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba.
Hatukuwatuma kwenda kuua Katiba na kutunga Katiba mpya. Kurekebisha ndiyo, lakini katika kurekebisha Katiba kuna mipaka yake.

Huwezi ukasema kwamba kwa kurekebisha Katiba, unaiua iliyopo na kutunga Katiba mpya. Ni sawa na kusema kiumbe kinaua muumba wake. Katika modern constituency jurisprudence hiyo haikubaliki kabisa. Lakini ilitokea hiyo mwaka 1965.
Katiba ya tano ambayo ni Katiba ya 1977 tuliyonayo sasa ina historia inayovutia.
Chimbuko la Katiba ya 1977 ni mapatano ya Muungano, ibara ya saba ya mapatano hayo ilisema kwamba Rais kwa makubaliano na Makamu wa Rais ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar, ataunda tume ya Katiba ikifuatiwa na kuitisha Bunge la Katiba ili kutunga Katiba ya Muungano katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Katika muda huo Katiba ya kudumu haikutungwa na baada ya hapo walijiongezea muda bila ukomo. Kwa hiyo, tukatawaliwa na Katiba ya muda ya 1965 kwa miaka kama 12 hivi.
Mwaka 1977 mchakato wa kuunganisha ASP na TANU ukaanza hatimaye halmashauri za vyama hivyo viwili zikakaa pamoja kukawa na chama kimoja-CCM.
Mara baada ya kuwa na chama kimoja mchakato wa kutunga Katiba ya nchi ukaanza. Mapatano ya Muungano yalisema kwamba Rais akikubaliana na Rais wa Zanzibar ataunda tume ya Katiba na Bunge maalumu.

Halmashauri ya Chama CCM ikapeleka kwa Mwanasheria Mkuu, ikatangaza katika gazeti la Serikali tarehe 4/4/1977 na Bunge maalumu likakaa tarehe 25, baada ya siku 20.
Wananchi hawakutoa maoni yao, hata wana-CCM hawakushiriki kwa sababu chombo kikuu cha chama ni Mkutano Mkuu, haukuhusika, iliyohusika ni Halmashauri Kuu ambayo mijadala yake ni siri.
Kwa hiyo Katiba ya 1977 wananchi hawakushiriki wala kushirikishwa na kutoa maoni yao. Katiba ya 1977 haina uhalali wa kisiasa; pili uhalali wake wa kisheria pia una walakini kwa sababu taratibu kuna sehemu zilifuatwa, lakini sheria zilipindwa. Kwa maoni yangu, Katiba zote wananchi hawakushirikishwa.

Je, utawala wa Nyerere halali?
Lakini hapa nitoe angalizo. Je, hii ina maana kwamba utawala chini ya Mwalimu Nyerere haukuwa na uhalali? Hapana, utawala wa Mwalimu Nyerere ulikuwa na uhalali.
Uhalali wake haukutokana na Katiba. Uhalali wake ulitokana na itikadi ya chama, umahiri na umaarufu wa Mwalimu mwenyewe.
Na tusichanganye, Mwalimu alikuwa anapendwa na watu wake, kwa hiyo utawala wake ulikuwa na uhalali wake ambao hata hivyo haukutokana na Katiba.
Medani ya kujenga muafaka haikuwa Katiba, ilikuwa chama ndiyo maana ya chama kimoja. Wananchi hawakujali Katiba. Kwa mfano, ukiwauliza kuhusu Azimio la Arusha walilijua sana na kulisherehekea lakini ukiwauliza Katiba hawakuijua.

Ndiyo maana Mwalimu alidiriki kusema; Katiba inanipa uwezo mkubwa sana hata kuwa dikteta.
Mara nyingi najiuliza, wananchi wake walisemaje waliposikia? Je, wananchi wasingesema du! kuna Katiba mbaya kiasi hicho? Wasingesema hivyo. Wangesema alhamdulilai tuna kiongozi mzuri.
Kwa nini? Kwa sababu wananchi hawakutaja Katiba na hii ilikuwa enzi za chama kimoja lakini ukiwa na vyama vingi medani ya kujenga muafaka haina budi iwe Katiba, si sera za chama. 

Mapendekezo ya mchakato
Tunapozungumzia Katiba mpya lazima kuwe na uhalali wa kisiasa na kisheria. Wananchi wanashiriki kikamilifu ili hatimaye wapate Katiba yao.

Mchakato uhakikishe wanapewa nafasi na muda wa kutosha kujadili mambo makubwa ya taifa kama dira, muelekeo, mustakabali wa nchi, mifumo yake kiuchumi na kisiasa, matakwa na maslahi ya wengi wanyonge. Wajadili katika mazingira huru bila kutishwa au kuzingirwa.
Napendekeza njia mbili. Moja, stage (jukwaa) ya kisiasa kujenga muafaka wa kitaifa.  Pili; stage ya kisheria kupitisha Katiba yenyewe, ili iwe na nguvu za kisheria.
Jukwaa la kwanza lianzie kwenye mijadala midogo kote nchini, iandaliwe na wananchi wenyewe katika taasisi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, ushirika, vyama vya kitaaluma, vijijini na mijini.
Mijadala hii midogo hatimaye itafikia kikomo chake katika mkutano mkuu wa kitaifa (National Convention). Hili ni jukwaa la kwanza.

Jukwaa la pili (la kisheria) linaanzia kwenye Bunge na kuishia kwenye kura ya maoni. Vyombo vikuu vitakavyohusika ni chombo cha kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na kuwawezesha kushiriki mijadala, tunaweza kuiita Tume, Rais ametangaza ataiunda, sina tatizo na hilo.
Lakini nina masuala matatu. Kwanza, tume hii itakuwa na majukumu gani... hadidu za rejea? Pili, itaundwa na watu gani? Tatu, taarifa yake au mapendekezo yatapelekwa wapi?
Hapo Rais hakufafanua, alisema majukumu ya tume ni kukusanya maoni na mapendekezo yatapelekwa vyombo husika. Hii inanipa shida kidogo.
Kama majukumu ya tume ni kukusanya maoni na kuwezesha mijadala...tume ambayo haina uwezo wa kufanya uamuzi haina haja iwakilishe interests (makundi) mbalimbali.
Kwa sababu ukiunda tume yenye kazi ya kukusanya maoni na kuwezesha mijadala, kuichambua na kuianisha maeneo makubwa ya msingi na kutoa muelekeo wake, tume hii iwe ya watalaamu ambao si wakereketwa wa vyama vya siasa.
Tume iwe huru kuendesha mijadala na hatimaye mapendekezo yake yapelekwe kwenye National Convention (mkutano wa kitaifa) itakaouandaa.

Rais amesema tume itapelekea mapendekezo yake kwa vyombo vinavyohusika....sasa hivi ni vyombo gani?
Hakuna vyombo vinavyohusika isipokuwa National Convention itakayokuwa na wajumbe kutoka makundi mbalimbali, taasisi za dini, NGOs na mkutano huu utajadili taarifa ya tume na baada ya kukubaliana, itatoka misingi mikuu ya Katiba - National Charter.

National Charter itakuwa na vision na misingi mikuu, ndiyo itakuwa na mwongozo wa watalaamu katika kuandaa rasimu ya Katiba na rasimu hiyo itaandikwa na jopo la watalaamu waliochaguliwa na mkutano wa kitaifa, si Mwanasheria Mkuu...haiwezekani.
Haiwezekani kwa sababu haitakuwa na mantiki kwa upande mmoja tume hiyo ya watalaamu wanaandika rasimu ya Katiba kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na mkutano mkuu wa kitaifa.
Kwa upande mwingine, Bunge kwa mujibu wa ibara ya 98 linapitisha sheria ya  kuwapo Bunge Maalumu la Katiba na sisi wananchi tutawachagua wajumbe wa Bunge Maalumu bila kujali vyama.
Bunge hilo litajadili kwa kina ibara za rasimu lakini lazima tukubaliane Bunge hilo la Katiba halitakuwa na kazi ya kupitisha Katiba kwa maana ya kuipa nguvu za kisheria.
Baada ya hapo (Bunge kujadili rasimu si kupitisha) Katiba itawekwa hadharani na itapigiwa kura ya maoni na kuwa Katiba rasmi ya nchi.
Kitendo cha wananchi kupiga kura kuhusu Katiba mpya ndiyo kitaipa nguvu ya kisheria. Kwa hivyo wananchi watakuwa wamepitisha Katiba yao na hivyo Katiba haitasema sisi Bunge maalumu tumetunga Katiba hiyo kwa niaba ya wananchi...hapana. Katiba itasema sisi wananchi wa Tanzania....

Jenerali Ulimwengu
Baada ya Shivji ilikuwa zamu ya Jenerali Ulimwengu ambaye alisema ya kuwa mjadala huo ni fursa ya kuandika Katiba mpya, kama alivyosema Issa (Prof. Shivji) si kwamba sababu kubwa ni Katiba hii ina upungufu. Hata hiyo mpya inaweza kuwa na upungufu.
Ni vizuri tukasema pamoja na upungufu huo nchi yetu imeendelea kuwa na amani hata kama siku hizi kidogo hiyo amani inaweza kuwa na .....lakini kwa ujumla tukilinganisha na wenzetu (nchi nyingine) wako ICU sisi tupo Kibasila (wodini Muhimbili).

Mtu wa Kibasila wakati anataraji kurudishwa nyumbani wa ICU watu wanafanya mipango (ya mazishi).
Mtu mwenye busara ni yule anayeamka asubuhi na kujisikia mzima (kiafya) halafu anampigia simu GP wake (daktari wake) anamwambia nataka nikuone. Daktari anamuuliza una matatizo gani? Anamwambia sina tatizo.
Sasa kwa nini unataka kuoniona? Nataka kukuona ili uniangalie hali yangu ilivyo nzuri leo halafu, unichunguze uniambie ni vitu gani ambavyo vinatoa dalili ya kunisumbua miaka 10 ijayo.
Huyo ndiye mtu mwenye busara ambaye angependa kuendelea na hali nzuri ya afya aliyonayo lakini anataka mtaalamu amwangalie na amwambie, katika miaka 10 ijayo usipoacha kuvuta sigara, kunywa pombe na usipofanya mazoezi utakuwa na kisukari au shinikizo la damu.

Ndiyo hali yetu leo na tusiseme tunaamka asubuhi tuna afya nzuri. Matatizo yameanza kujitokeza. Kuna hali kidogo ya kutoelewana kama tulivyozoea kuelewana. Ni ishara kwamba; wakati ndiyo huu.
Baada ya kupata Uhuru na makubaliano baada ya wakuu wa dola ya Uingereza na viongozi wakuu wa mapambano ya kutafuta huru, si hapa Tanganyika na baadaye Tanzania, bali karibu nchi zote za Afrika, kumekuwa hakuna mchakato uliofuatilia hatua ya Uhuru.
Mchakato wa kuwaambia wananchi tuketi chini Uhuru ni huu tunao sasa tunafanya nini, namna gani tuendeshe nchi yetu. Imekuwa ni mchakato unaofanyika ndani ya chama tawala au kwa kutumia wataalamu au tume iliyoteuliwa na wakuu wa chama tawala na hao ndiyo waliofanya kazi ya kubandua na kubandika vifungu vya Katiba.

Hata kwa wataalamu tu wakati mwingine ni vigumu kujua kipengele kimoja cha Katiba kinawiana vipi na kipengele kingine.
Kwa mfano, sasa hivi nani anajua ni namna gani Katiba mpya ya Zanzibar inavyohusiana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano?
Kama kuna mtu ameyaona anipe nakala lakini kuna vipengele vingi ndani ya Katiba yetu vinamatatizo na haviwiani.

Kwa mfano, je, tunajua Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania...na hapa kuna matatizo hatujui hata jina lenyewe ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au ni Jamhuri ya Muungano ya Tanzania?
Hata hilo hatujui, ingekuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kenya...sawa lakini kama ni Tanzania peke yake basi ni Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mpaka sasa hakuna mabadiliko ya Katiba yenye manufaa kwa wananchi, kwa mfano mwaka 1990 hadi 1995 nilikuwa mbunge, tulibadilisha vipengele fulani ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
Kama mnavyojua chama tawala hakikupenda kuwapo vyama vingi, vilikuja kwa sababu kimsingi hali ilibadilika duniani, ilikuwa haistahimiliki tena kuwa na mfumo usioruhusu watu kuunda vyama kama wanavyopenda na msukumo binafsi wa Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa muhimu sana.

Nilikuwako Diamond Jubilee wakati Mwalimu Nyerere anatoa hotuba yake, mwaka 1991 na kwa mara ya kwanza na ya mwisho, nimeshuhudia Mwalimu Nyerere anazungumza katika mkutano wa CCM, chama chake alichokiasisi, halafu watu wanaguna (kupinga vyama vingi).
Jambo hilo limetufundisha kwamba ndani ya chama tawala hawakupenda mfumo wa vyama vingi na wameuwekea vikwazo kila wakati.
Hata pale ambapo wamefanya mabadiliko yenye manufaa kwa umma, imekuwa ni alimradi wakidhi haja ya muda fulani na kuibana baadaye.
Kwa mfano, mwaka 1992 nikiwa mbunge tumeondoa kipengele kinachomruhusu Rais kuteua wabunge. Tukafanya uchaguzi wa mwaka 1995 Bunge likawa la watu wa kuchaguliwa ukiacha viti maalumu vya wanawake.
L
akini mwaka 2000 vimerejeshwa viti vya Rais, kwa maana ukiweka viti 10 vya Rais na wakuu wa mikoa, ukaweka na mawaziri na manaibu mawaziri wote ni wabunge, Bunge lako unakuwa umelikata kwa zaidi ya theluthi moja. Si Bunge tena, ni wawakilishi wa serikali. Haya yanakuja ili kukidhi mahitaji ya muda.
Kama walivyosema wawakilishi wa serikali kwani mna tatizo gani na Katiba? Kila tunapoona kuna haja tunanyofoa moja, tunaweka nyingine. Hii niliipenda kwa sababu walikuwa wakweli.
Sasa hii tuliyoiweka mpya kama haiendani na kifungu kingine ambacho bado kimo kwa sababu hatukukinyofoa hatukioni kwa sababu kimoja tumekinyofoa na kingine kinyume cha kunyofoa...kunyofeka.
Na kwa sababu ya mahitaji ya muda wakati ule mwaka 2000 ni hizi; Bwana Mkapa nilifanya kampeni yake mwaka 1995, tukapata taabu sana kwa Augustine Mrema na Mabere Marando, tuseme ukweli.
Kwa sababu ya taabu tuliyoipata uchaguzi wa 1995 na kwa sababu ya Bwana Mkapa kutojiamini kwa uchaguzi wa 2000, na kwa sababu Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge, alikuwa tayari kumfanyia Mkapa vitu anavyotaka, wakakubaliana mabadiliko ya sheria kupelekwa bungeni.

Wakanyofoa na kunyofeka mabadiliko, kipengele ambacho leo wamesahau kukiondoa. Mtu anaweza kuchaguliwa Rais hata kama amepata asilimia 19, alimradi ndiye mwenye kura nyingi kuliko mwingine.
Kwa hiyo unaweza kuwa na Rais ambaye umaarufu wake ni asilimia 19, kisa tulimwogopa Mrema.
Mambo haya ya kubadilisha kipengele cha Katiba kwa sababu ya mtu fulani, au uwoga fulani au kwa sababu ya maslahi fulani ndiyo yanayotufanya tukatae hoja zozote za marekebisho ya Katiba zinazotokana na political expediency kutaka kupata faida haraka...kesho.
Katika vyama vya upinzani wangetaka vipengele vibadilishwe haraka ili uchaguzi ukija kesho wakiondoe madarakani CCM. Sidhani kama hilo ndilo lengo letu. Tujipe muda wa kujenga Katiba mpya inayokidhi mahitaji ya Tanzania.
Wananchi wanaweza kujadili Katiba yao kama tunajipanga vizuri.
Kama Rais ametangaza ataunda tume ya kuratibu maoni, basi iwe tume ya kuratibu maoni, kupanga na kuweka mpangilio wa uratibu wa mijadala ya kina na iliyoenea nchi yote.
Sikubaliani na mheshimiwa anayesema shughuli ya kuandika Katiba ina gharama kubwa sana. Kama ina gharama hebu tuangalie gharama walizoingia Wakenya kabla ya kuandika Katiba yao.
Hakuna gharama kubwa sana kuliko machafuko yanayoweza kutokea kwa sababu hamjaelewana vizuri ni namna gani ya kutawala nchi yenu.

Tunahitaji kupigania ushirikishwaji wa wananchi si vyama vingi. Washiriki na kuamua namna gani mali zao, zinawanufaisha, wawe na madaraka juu ya maisha yao.
Ili kesho CUF, CHADEMA wakiingia Ikulu au CCM ikibaki Ikulu no big deal  (hakuna cha mno) kama haya mambo yanayohusu wananchi moja kwa moja yaameangaliwa.
Mambo hayo ni kwanza; raia kuwa na nafasi juu ya serikali, si siasa za vyama au serikali kuwa juu ya raia.
 
Leo unataka kuandamana halafu polisi anasema huwezi. Kwa nini? Kwa sababu nadhani utafanya fujo.
Maandamano ni pamoja na kuandamana kumuunga mkono Rais kwa sababu ametoa tamko zuri, au kumpinga kwa sababu ametoa tamko baya. Sasa kwa nini uruhusu upande mmoja na uzuie mwingine?
Ni dalili kwamba utawala wetu bado una kitovu kilichoshikiliwa na mifumo ya ukoloni. Na haishangazi kwa sababu ndiko tulikotoka na tumeshindwa kuchukua hatua za dhati za kukata kitovu hicho.
Njia iliyopo ni kukutana sote katika makongamano kama haya kwa amani, utulivu, kuheshimiana na kupunguza jazba.

Kuwe na utangamano kati ya Serikali, Bunge, wanasiasa, wananchi wa kawaida, vyombo vya habari, waumini wa dini mbalimbali, akina mama, vijana, wafanyakazi, wapiganaji, wanausalama ni muhimu sana, tuwe nao ili kuweza kuwaambia kuwa ninyi hamtutawali sisi, nyie ni watumishi wetu na waelewe hivyo.
Mchakato huo uwahusishe wote na kila mtu ajue nafasi yake. Polisi hawezi kuwa mtawala wa wananchi isipokuwa polisi wa kikoloni. Polisi ni mtumishi wa wananchi hilo liandikwe sawasawa na lijulikane.
Nashukuru Rais ameliona hilo. Kusema tu nitashughulikia ni muhimu, lakini isije ikawa imetolewa fursa kwa mkono mmoja na kuondolewa kwa mkono mwingine.
Kama ikitokea wananchi hawajaridhika na mchakato utakaotumika kutunga Katiba mpya, hakuna sababu ya kuacha kufanya kampeni.
Tutaendelea kufanya kampeni kwa sababu sidhani hii Katiba inaweza kukamilika katika miaka mitatu ijayo nadhani hata miaka mitano ni michache.

Hii ni nafasi ya Tanzania kujiumba upya, kujisanifu upya, tunahitaji muda. Tusijaribu kufanya mchezo wa kumuwahi mwenzako.
Katika majanga makubwa yaliyoipata nchi hii ni fasta-fasta (harakaharaka), hili si zoezi la asasi moja.
Haliwezi kuwa zoezi la Rais wa Jamhuri, Bunge, vyama vya siasa, wala zoezi la jopo la wanazuoni au waandishi wa habari. Ni zoezi la wote, kila mmoja kwa nafasi yake, Rais ana nafasi yake kutuongoza.
Ndiye mkuu wetu, anaweza kuunda tume sina tatizo na hilo, vyama vya siasa vina haki ya kutoa maoni yao na kuunganisha wananchi wake washiriki mjadala.

Wanazuoni mnaweza kutuongoza katika vipengele muhimu tusije kuvisahau. Bunge wakati ukifika litakuwa na nafasi yake lakini muhimu kuliko yote ni wananchi wote.
Si dhima ya serikali kudhamini muendelezo wa mapokeo ya kidemokrasia (democratic tradition). Serikali yoyote duniani, kazi yake ni kukamata, kudhibiti.
Hakuna serikali ambayo kwa silika ya serikali inaendeleza mapokeo ya demokrasia, lazima ipigwe shinikizo ndiyo iendeleze mapokeo ya demokrasia.

Serikali inayoongozwa na watu wenye busara huwa inasoma ishara za nyakati. Na wengi wanasema maandishi ukutani huwa hayaandikiki kwa mara moja.
Huanza herufi moja moja, kabla ya kujitokeza neno lote, inaweza kuanza M, inakuja A halafu P, sasa ikifika P unaweza kusema ni Mapinduzi kwa hiyo unachukua hatua. 
Kwa hiyo serikali inayoongozwa na watu wenye busara, wanaojua historia ya dunia inajua ni wakati gani kuchukua hatua.
Mdhamini mkuu wa muendelezo wa mapokeo ya demokrasia ni asasi za kijamii, kazi ya vyama vya kijamii si kuchukua nafasi ya serikali bali ni kuistaarabisha serikali kwa kuishinikiza kila wakati kuwaambia mkifanya hivi mnatuumiza.

Tuangalie masuala makuu yafuatayo. Kwanza mjadala wenye usawa ili kuwa na taifa lisilokubali utajiri mkubwa uende kwa kundi dogo wakati wananchi wengi wanadidimia kwa umasikini.
Taifa linalojiuliza maswali kama haya; rasilimali za Taifa ni za nani? Ni mali ya serikali, wawekezaji au wananchi? Zitumike vipi, zimnufaishe nani, kwa kiasi gani na kwa sababu gani?
Nani awe na kauli ya uzito wa kiasi gani kuhusu rasilimali hizi na kwa sababu gani. Jamii zinakoishi huko zinakopatikana rasilimali zina haki zipi za msingi na wajibu gani wa kutimiza.
Mambo kama Loliondo na kwingine ambako kwa sababu tu ardhi waliyonayo wananchi ina rasilimali fulani basi wao ndiyo wanakuwa kero.

Nimesikia wakuu wa serikali wakionya halmashauri msipofanya haya tutafuta hii halmashauri kwa hiyo kuwapo kwa halmashauri za wilaya na miji ni kwa hisani ya serikali kuu. Hii haitakiwi, zinatakiwa kuwapo serikali kuu ipende, isipende.

Je, bado iko haja ya wakuu wa wilaya na mikoa wanaoteuliwa Dar es Salaam? Huu ni utaratibu mwingine wa ukoloni. Gavana alikuwa anakaa Dar es salaam na anateua wawikilishi wake.
Siku hizi wakuu wa wilaya na mikoa sijui wanateuliwa kwa misingi ipi. Ukitazama wakuu wa wilaya, utakuta mhitimu wa darasa la saba na mwenye PhD. Halafu kuna koplo na Brigedia General, wote wakuu wa wilaya.
Mtu amezaliwa Muheza anakuwa mkuu wa wilaya alete maendeleo Nkasi, halafu imefika mahali mpaka wananchi wanajua huyu kaletwa hapa kwa sababu ni shemeji ya aliyeko huko juu.
Halafu imefikia hata wachumba zenu wanakuwa wakuu wa wilaya. Haya ni mambo ya kujadili na wananchi kuchagua wakuu wao katika nafasi za kisiasa kama wakuu wa wilaya.
Katika masuala ya kuendeleza kilimo cha wananchi wa Mtwara au Sikonge au Karagwe nadhani tuanze kuzungumza hili suala, tujadili kama umuhimu kuanza kuwachagua wakuu wa wilaya.

Je, bado tunahitaji wabunge 230 na zaidi? India wapo karibu watu bilioni moja lakini wana wabunge 500 tu, sisi wananchi milioni 40 tu wabunge wote hao?
Je, tunataka nchi yenye mfumo wa kibunge (parliamentary system) au mfumo wa Rais mtendaji (presidential system). Sasa hivi tuna mfumo koko, haujulikani.

Kuna wakati, siku moja miaka ya ‘70 Mwalimu aliulizwa kwa nini unateua mtu katika nafasi ambayo haiko kwenye Katiba, kwamba unamteua Waziri Mkuu.
Mwalimu akasema haikuandikwa kwenye Katiba kwamba kutakuwa na Waziri Mkuu lakini vile vile haikuandikwa kwamba hakutakuwa na Waziri Mkuu.
Kwa hiyo, kimsingi watu wetu ni wema lakini watawala ovyo, matokeo yake tumejenga jamii ya watu wengi wasioaminika, matapeli, wababaishaji na wapuuzi.
Tumekubali wito wa kuwa mjanja, chizika, pata mzuka, full - kujirusha ambayo yote yametujaza upuuzi wa kibambucha. (Tumekuwa) Jamii isiyopenda kujifunza, tumevifanya vitabu kama wakwe zetu, tunaogopa kuvifunua.
Watu wa kutoa majibu mepesi kwa maswali mazito kwa sababu hatupendi kusumbua akili zetu, wapiga kura wanaouza kura zao kwa bakuli la kunde, kisha wanalalamika kukosa uongozi bora.
Imefika mahali tunamwadhibu mwizi wa kuku lakini mwizi mwingine anachaguliwa mbunge. Ni jamii iliyopotea ambayo haiwezi kuandika Katiba.
Fanya unavyotaka hutapata cha maana kwa sababu humo ndani kutakuwa na wezi wazandiki, wala rushwa, kila mmoja anajaribu kuweka maslahi yake mbele kwenye katiba mpya.
Kwanza, tuanze kupambana kujenga maadili kabla ya Katiba mpya na nadhani wanasiasa wameshindwa kazi hii, pengine tuwageukie viongozi wa dini watasaidia.
Ili kupambana na haya niliyoyasema ambayo ni majanga makubwa yanayotawala, turudi kwenye misingi ya Uhuru. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu kuondoa umasikini, ujinga, maradhi na dhuluma...ongeza na rushwa.

Sitapokea wala kutoa rushwa, cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cheo cha mtu mwingine kwa faida yangu. Hebu niambieni watu gani wa serikali wanaweza kujitokeza hadharani na kusema maneno haya.
Sasa tuwafanye wayaseme haya (katika katiba mpya). Katika mchakato wa kujadili Katiba mpya tufike mahala tuwalazimishe watu walioko kwenye utawala waseme hivi; cheo ni dhamana sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa manufaa yangu, waseme halafu tuwapime.
Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya nchi. Nasikia wanafunzi wengi sana mnasoma accoutancy (uhasibu) ni somo zuri lakini sijui mnataka kwenda kufanya kazi wapi?
Nitashirikiana na wenzangu kujenga nchi yetu, nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko. Raia mwema wa Tanzania, Afrika na dunia nzima tuyatafakari haya, tuwe na muafaka wa kitaifa, tuwe na national charter kutokana na hilo.
 

No comments: