Na Maggid Mjengwa,
SEPTEMBA 11 mwaka huu ulimwengu utaadhimisha miaka kumi tangu kutokea kwa shambulizi kubwa la kigaidi nchini Marekani. Hakika, tangu hapo, hofu ya kutokea matukio ya ugaidi imeongezeka duniani. Na ajabu ya matukio ya ugaidi, kihistoria, mengi ya matukio makubwa ya ugaidi humu duniani yamefanyika katika mwezi wa Septemba. Kwanini?
Ni ukweli wa kihistoria, kuwa mwezi Septemba ni mwezi wenye kuambatana sana na matukio ya kigaidi. Mfululizo wa simulizi hii utakupa wewe msomaji, mwanga na maarifa juu ya mambo ambayo hukuyajua juu ya ugaidi wa kimataifa, aidha, utakupa nafasi wewe msomaji uliyefahamu kabla kukumbuka juu ya kile ulichokijua kabla.
Kupitia simulizi hii utapata pia kufahamu na kuona juu ya mahusiano ya mwezi Septemba na ugaidi wa Kimataifa. Juu ya hapo, ni imani yangu kuwa simulizi hii itakufanya uburudike na kufurahia kusoma.
Naam, Kwa faida ya wasomaji, nitaanza kwa kuangalia chimbuko la ugaidi wa kimataifa kwa kuangalia chimbuko lake kihistoria. Katika kulifanya hilo nitatoa mifano mbalimbali.
Ni rahisi kusema kwamba ulimwengu umebadilika baada ya ugaidi wa Septemba 11 mwaka 2001 kule nchini Marekani. Kwamba ugaidi umesogea karibu zaidi katika fikra zetu. Watanzania bado tunakumbuka tukio la shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la ubalozi wa Marekani jijini Dar Es Salaam. Ilikuwa ni Agosti 7, 1998.
Sura ya ugaidi wa kimataifa imeonekana vema zaidi miongoni mwa walimwengu. Bila shaka, picha ya filamu ya televisheni yenye kuonesha majengo mawili ya World Trade Centre kule Marekani yakitunguliwa na kuanguka, zimeonwa na takribani asilimia 75 ya watu wa ulimwengu huu. Katika hili la kuchambua ugaidi, hebu basi tuanze na kujiuliza;
Ugaidi ni nini?
Itakumbukwa, kuwa mwaka 2003 wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikutana Dodoma na kupitisha Muswaada wa Ugaidi. Waheshimiwa wabunge wale walitumia muda mwingi sana kujadili tafsiri ya neno "ugaidi".
Kwa kifupi, ugaidi ukitafsiri kutoka neno la Kiingereza "Terrorism" tunapata maana ya "hofu". Neno la Kiingereza "Terror" lina maana ya hali ya "kutisha". Vitendo vya kigaidi hutumiwa na mtu au makundi ya watu ili kuwaingizia watu hofu ndani ya mioyo yao na pengine hata kuchukua madaraka ya kisiasa. Ugaidi ni njia ya mnyonge na hata mwenye nguvu kutimiza malengo yake. Hili litafafanulika zaidi kadri utakapofuatilia maandiko haya.
Kihistoria tunaona kuwa, vitendo vingi vya kigaidi humu duniani vimefanywa pia na dola zilizo madarakani kwa minajili ya kuendelea kushika hatamu za dola. Mathalan, msemo wa " Utawala dhalimu" kwa tafsiri ya Kiingereza "Terror regime" hutumika tunapoielezea dola yenye kutumia mabavu na nguvu nyingi kupita kiasi. Dola au mtawala asiyezingatia sheria wala haki za kibinadamu.
Msamiati huu wa utawala dhalimu unatokana na lugha ya Kifaransa na una chimbuko la Mapinduzi ya Wananchi kule Ufaransa kati ya mwaka 1789 hadi 1799. Utawala dhalimu wenye kutisha" la terreur" ulikuwapo kule Ufaransa kunako miaka ya kati ya 1792 hadi 1794. Katika kipindi hicho watu takribani 40,000 wengi wao wakiwa wakulima na wahunzi waliuawa.
Mifano ya tawala dhalimu na za kutisha katika sehemu nyingine za dunia ni kama Urusi ya zamani chini ya dikteta Stalin, utawala wa Kinazi wa Ujerumani kati ya 1933-1945 chini ya Fashisti Hittler. Katika Afrika, tuna pia mifano kadhaa ya tawala dhalimu na za kutisha, tawala ambazo kimsingi ni za kigaidi. Uganda ya Idi Amin, Afrika ya Kati ya Bokassa, Zaire ya Mobutu ni kati ya mifano michache miongoni mwa mingi.
Ugaidi kimsingi ni ile hali ya mtu, kikundi au dola kwa maana ya taifa kutumia nguvu nje ya wigo wa sheria ili kufikia malengo yao. Mwenye kuendesha vitendo vya kigaidi huchagua watu wake watakaoathirika na vitendo hivyo. Si lazima mtu au watu hao watakaoathirika wawe ni wahusika wa moja kwa moja wa mgogoro husika, isipokuwa waathirika mara nyingi huchaguliwa na huonekana kama wawakilishi wa malengo ambayo magaidi wanataka kuyafikia. Malengo au sababu za ugaidi zaweza kuwa ni za kidini, kijamii na kisiasa.
Ugaidi huwa wa kimataifa pale tukio la kigaidi linapofanywa nje ya mipaka ya yule anayatenda tendo la kigaidi, au raia wa nchi moja wanapokuwa walengwa na kuathirika na tendo la kigaidi katika nchi ya tatu, mathalani magaidi kutoka Saudi Arabia wanapofanya tendo la kigaidi dhidi ya raia wa Uingereza katika nchi ya Zambia. Je, kuna makundi ya kigaidi ya aina ngapi? Simulizi hii itaendelea...
No comments:
Post a Comment