To Advertise on this Blog please Call: O713 397 767 or 0785 555 560                                                 To Advertise on this Blog please Call: O713 397 767 or 0785 555 560
Mail Me

Thursday, December 15, 2011

Matokeo STD VII Yatangazwa, Watahiniwa 567,567 Wafaulu, 9,736 Wafutiwa Matokeo

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (kushoto) akitangaza matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika nchini mwezi Septemba 2011 jana jijini Dar es Salaam. Katika matokeo hayo wanafunzi 567,567 kati ya 983,545 wamefaulu mtihani huo, wavulana wakiwa ni 62.49% na wasichana wakiwa 54.48% ufaulu ukiongezeka katika masomo ya kiingereza, Kiswahili, Maarifa ya Jamii, Sayansi na Hisabati huku wanafunzi 9736 wakiwa wamefutiwa matokeo yao mkoa wa Manyara ukiongoza. (Picha na Aron Msigwa –MAELEZO)

Na Gradys Sigera na Magreth Kinabo – MAELEZO
JUMLA ya wanafunzi 567,567 wamefaulu Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Mwaka 2011, na sasa watafanyiwa mtihani wa majaribio kabla ya kuanza masomo yao katika shule walizochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, ili kubaini wadanganyifu.

Akitangaza matokeo hayo, jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (Mb) amesema, utaratibu huo wa kufanyiwa majaribio utaanza mwakani 2012, ambapo wanafunzi waliofaulu watafanyiwa majaribio ya kupima stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Wakati huo huo, Baraza la Mtihani la Taifa limefuta matokeo yote ya watahiniwa 9,736 sawa na asilimia 1.0 waliobainika kufanya udanganyifu wakati wa mtihani huo.

“Mwanafunzi atakayebainika kuwa kajiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo, Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Waziri Mulugo.
Akizungumzia kuhusu kiwango cha ufaulu alisema kimeongezeka hadi kufikia asilimia 58.28 ukilinganisha na cha mwaka jana ambacho kilikuwa asimilia 53.52.
Aliongeza kuwa kiwango cha ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hesabu kimepanda. Somo la Kiingereza kutoka asilimia 36.47 mwaka jana hadi asilimia 46.70 kwa mwaka huu, wakati somo la Sayansi ni asilimia 61.33 mwaka huu toka asilimia 56.05 mwaka jana na Hesabu asilimia 39.36 mwaka huu toka asilimia 24.70 mwaka jana.
Jumla ya wanafunzi 983, 545 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwezi wa Septemba 2011 na kuonesha kuwa, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 53.52 mwaka jana hadi 58.28. Jumla ya wasichana waliofaulu ni 27,377 na wavulana ni 289,190.

Wakati huo huo, Serikali imesema, kazi ya kuhakiki madai ya walimu imekamilika tangu Desemba 2, mwaka huu na kwamba madai hayo ni kiasi cha sh. bilioni 52.
Akijibu swali lililoulizwa na waandishi kuhusu madai ya walimu, Naibu Katibu Mkuu, Selestine Gesimba amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 30 ni za mishahara na bilioni 22 ni za madai mengineyo.
Gesimba ameongeza kuwa, madai ya malipo mengine yataanza kulipwa mwezi huu (Desemba) na madai ya malipo ya mishahara yatalipwa ifikapo Januari 2012. Hata hivyo alisema tayari Hazina wameshalipa bilioni 28 za madai ya mishahara kuanzia Julai mwaka jana hadi Novemba mwaka huu.

No comments: