SIKU tatu kabla ya uchaguzi mdogo wa Igunga, viongozi vijana wa CCM na Chadema wamefikia muafaka wa kusuluhisha migongano kati ya mashabiki wa vyama hivyo.
Muafaka huo umetokana na mazungumzo kati ya vijana hao yaliyofanyika jana katika hoteli iliyofikiwa na viongozi wa Chadema mjini hapa.
Akizungumzia muafaka huo, kada wa CCM, Hussein Bashe, alisema mazungumzo hayo yalianza Jumamosi kwa njia ya simu kati yake na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na wakakubaliana yafanyike Igunga.
"Tumefanya mazungumzo ya kirafiki tu ya kutuliza munkari wa vijana wetu," alisema Bashe katika mazungumzo na gazeti hili kwa njia ya simu.
Kutokana na mazungumzo hayo ya Jumamosi, jana baada ya helikopta ya CCM kutua katika viwanja vya Sabasaba, ikiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, January Makamba, vijana wa CCM walitaarifiwa waende katika kikao hicho.
Kwa mujibu wa Bashe, yeye na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Beno Malisa, walikwenda katika hoteli waliyofikia Chadema na baadaye walifuatwa na January na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilary (CCM).
Baada ya akina January kufika, vijana wa Chadema waliungana kushiriki mazungumzo hayo akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Lema na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche.
Wengine ni Mbunge wa Singida Magharibi, Tundu Lissu (Chadema), wabunge wa viti maalumu Chadema, Suzan Lyimo na Grace Kiwelu na Katibu Mkuu Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Uamuzi wa kikao Akizungumzia uamuzi wa mazungumzo hayo, January alisema wamekubaliana kuendelea kuzungumza kila panapotokea kutoelewana kati ya mashabiki wao na kila upande ujitahidi kuzuia jazba za vijana wao.
"Mimi nilisikitishwa sana na hali ya vurugu zinazoendelea hapa na katika kikao chetu, tumezungumza vizuri na kukubaliana kuwa ili tufanikishe kampeni na uchaguzi, tuondoe vurugu. Tumekubaliana tusiache makovu baada ya uchaguzi," alisema January.
Chadema ‘wamtaka’ Aeshi Wakati mazungumzo ya amani yakifanyika, vijana wa Chadema walikusanyika katika hoteli hiyo na kutaka viongozi hao wa CCM watolewe nje, ili wawashughulikie.
Vijana hao walikuwa wakilalamikia madai ya baadhi ya vijana wa CCM, kuwapiga vijana wenzao wa Chadema, waliokuwa wamehudhuria mkutano wa kupokea helikopta ya CCM. Katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wassira, aliuliza kama mashabiki wa Chadema walikuwa kwenye mkusanyiko huo na kuwataka wanyooshe mikono juu.
Baada ya mashabiki hao kuonyoosha mikono wakionesha alama ya 'V' ya chama hicho, baadhi ya vijana wa CCM waliwakamata baadhi yao na kuwaweka katika gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop na kuondoka nao.
Kwa mujibu wa taarifa za Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi, Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu, vijana hao wanashikiliwa Polisi kwa tuhuma za kufanya fujo katika mkutano huo.
Baada ya vijana wa Chadema kukusanyika kutaka wenzao warudishwe na kukuta kuna mkutano wa muafaka, wakataka waruhusiwe kumkabili Aeshi kwa madai kuwa ndiye adui yao.
Hata hivyo, Dk. Slaa aliingilia kati na kusema kuwa January na Bashe ni wastaarabu ila Aeshi ndiye aliyewavurugia na kuzungumza na vijana hao wasitishe vurugu.
January alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kuongeza kuwa zilihusu madai ya kurushiana risasi hivi karibuni kati ya Mratibu wa Kampeni za Chadema, Mwikwabe Mwita, Aeshi na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya wote wa CCM. Zitto aliwasifu na kuwapongeza Bashe na Lema kwa kubuni wazo la kutafuta muafaka wa Igunga.
No comments:
Post a Comment