Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na balozi wa Japan anayemaliza muda wake Mh. Hiroshi Nakagawa wakati balozi huyo alipokwenda ikulu jijini Dar es Salaam jana. |
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Mheshimiwa Nakagawa amemwaga Rais Kikwete baada ya kuwa amemaliza muda wake wa kuiwakilisha nchi yake ya Japan katika Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemshukuru Mheshimiwa Nakagawa kwa mchango wake mkubwa wa kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kusaidia kuongezeka kiwango cha misaada ya Japan kwa Tanzania.
“Nakushukuru sana kwa kukuza sana uhusiano baina ya nchi zetu wakati wa kipindi cha uwakilishi wako. Umesaidia sekta nyingi za maendeleo ya nchi yetu hasa kilimo na miundombinu. Tunajua kuwa pia hiki kilikuwa kipindi kigumu kwa Japan kwa sababu ya zahama ya tsunami,”Mheshimiwa Rais amemwambia balozi huyo na kuongeza:
“Kama unavyojua, Tanzania inaunga mkono jitihada za Japan kuwa mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini na sisi katika Afrika tunapenda kukumbusha kuwa bado tunaitaraji Japan kuunga mkono jitihada za Bara letu kupata nafasi mbili za ujumbe katika Baraza hilo. Kama unavyojua, Tanzania haiwanii kupata moja ya nafasi hizo. Sisi tunaridhika kutumikia katika nafasi ya ujumbe wa muda wa Baraza hilo.”
Naye Balozi Nakagawa amemshukuru Rais Kikwete kwa kumwunga mkono katika kipindi chake cha utumishi akisititiza kuwa baadhi ya mambo ya msingi yaliyofanyika katika kipindi chake mbali ya kuongezeka kwa misaada ya maendeleo kutoka Japan ni ziara ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda katika Japan na uandaaji wa pamoja wa Tanzania na Japan wa Mkutano wa TICAD mjini Arusha Mei mwaka jana.
Balozi Nakagawa ambaye amemwambia Rais Kikwete kuwa anarejea nyumbani kustaafu kwa mujibu wa sheria amesisitiza kuwa ataendelea kuwa rafiki wa Tanzania na atatafuta namna nyingine ya kusaidia maendeleo ya Tanzania nje ya utumishi wa umma katika Japan.
Balozi Nakagawa pia kwa mara nyingine amewasilisha salamu za rambirambi za Japan kwa Serikali ya Tanzania kufuatia ajali ya karibuni ya meli ya Spice Islander ambako watu 202 walipoteza maisha.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute). Ujumbe huo uliongozwa na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Finland Mheshimiwa Anne Sipilainen aliyefuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Joseph Semboja.
Bibi Sipilainen ndiye mwenyekiti mwanzilishi wa Bodi ya Uongozi Institute ina makao makuu yake hapa nchini na ambayo uendeshaji wake unachangiwa kwa pamoja na nchi za Tanzania na Finland.
Wakati wa mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais ameuelezea uongozi huo kuhusu visheni yake ya taasisi hiyo akisisitiza kuwa angependa kuwa taasisi hiyo iwe ya kanda ya Afrika na ilenge katika kutoa mafunzo kwa viongozi juu ya maendeleo hasa katika nyanja za Utawala Bora, Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii kwa namna ya kulenga kulitoa Bara la Afrika katika umasikini, masuala ya tabia nchi na utafiti.
No comments:
Post a Comment